Shein aagiza vyuo vikuu kusajili wenye sifa

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amevitaka vyuo vikuu nchini kuwa makini katika usajili wa wanafunzi wanaojiunga vyuoni humo, kwa kuhakikisha wanakidhi viwango vinavyohitajika katika ngazi za Taifa na Kimataifa.

Aliyasema hayo jana katika Chuo Kikuu cha Zanzibar kilichopo Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja katika katika Mahafali ya 14 ya chuo hicho.

Alisema hivi karibuni kumeibuka baadhi ya vyuo vinavyosajili wanafunzi bila ya kufuata viwango husika, jambo ambalo linaharibu sifa ya elimu na maendeleo ya wananchi na nchi kwa jumla, itakayoweza kusababisha kupata wataalamu wasiokuwa na sifa hapo baadaye.

Alisema kuwepo kwa ushindani mkubwa wa kutafuta wanafunzi wapya wanaotaka kujiunga katika vyuo vya ndani na nje ya nchi isiwe sababu ya kuharibu ubora wa elimu kwa kusajili wanafunzi wasio na viwango kuingia katika vyuo vikuu.

Aidha, alivitaka vyuo vikuu nchini kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakuwa na wahadhiri na vifaa vya kutosha sambamba na kuwa na uwezo wa kuendesha mafunzo hayo ili kuepuka kutoa elimu isiyokidhi haja.

Alisema mambo hayo kwa pamoja ni muhimu katika kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa Tanzania.

Alisema ubora wa elimu inayotolewa ni suala la ushirikiano kati ya jamii, vyuo na serikali na kuhimiza haja kwa vyuo vikuu vya Zanzibar kufanya kazi karibu zaidi katika kuhakikisha elimu inakidhi mahitaji yaliyokusudiwa na wanafunzi nao wanakidhi viwango.

Dk Shein alitumia fursa hiyo kuwataka wazee kuendelea na malezi bora ya watoto wao sambamba na kuwa karibu na maendeleo yao ya elimu huku akiwahakikishia kuwa serikali itaendelea kutoa elimu bure pamoja na kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa ya kujiunga na elimu ya juu.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alitoa pongezi kwa uongozi wa chuo hicho kutokana na kuendeleza utamaduni mzuri wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu, hatua ambayo imesaidia kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Profesa Saleh Idris wa chuo hicho, alisema wana azma ya kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya kwa kuanzisha Shahada ya Uuguzi ambayo wahitimu 53 ni miongoni mwa waliohitimu mahafali ya mwaka huu.

Published by Samcare Service

...Usiwaze Mabaya juu ya jirani yako. Ambaye anakaa karibu Nawe na kujiona Salama... "

Leave a comment